Pata chanjo ya COVID-19: Unachopaswa kutarajia | Getting your COVID-19 vaccine: what to expect

Chanjo ni mojawapo ya njia tunazoweza kupambana na janga la COVID-19 na kulinda afya na ustawi wa jamii zetu.

Kinga

Chanjo za COVID-19 hazilipishwi na zinapatikana kwa kila mtu nchini Nyuzilandi.

Chanjo hulinda afya yako na huzuia magonjwa kwa kufanya kazi na kinga asili ya mwili wako ili uwe tayari kupambana na virusi, ikiwa utaambukizwa.

Chanjo ya COVID-19 hufanya kazi kwa kuchochea mfumo wako wa kinga kutoa kingamwili na seli za damu zinazofanya kazi dhidi ya virusi vya COVID-19.

Kupata chanjo ya COVID-19 ni hatua muhimu unayoweza kuchukua ili kujikinga na athari za virusi.

Mara baada ya kupata chanjo, endelea kuwa mwangalifu kuzuia COVID-19 kuenea. Nawa kabisa na ukaushe mikono yako. Kohoa au upige chafya ukijifunika na kiwiko chako na ukae nyumbani ikiwa unajihisi mgonjwa. Hii itakusaidia kujikinga, whānau wako na wengine.

Endelea kutumia programu ya ufuatiliaji wa COVID, washa Bluetooth kwenye simu yako, na unaweza kuvaa kifunika uso au barakoa.

Usalama

Medsafe hutoa kibali kwa chanjo kutumika nchini Nyuzilandi ikiwa tu wameridhika kuwa ni salama na yenye ufanisi wa kutosha kutumika. Chanjo zote za COVID-19 zitapitia jaribio hilo la usalama na lazima zitimize viwango sawia.

Chanjo ya Pfizer

Chanjo hii haitakupa COVID-19. Utahitaji vipimo viwili, angalau vikiachana kwa wiki tatu. Ili kuhakikisha una kinga bora, hakikisha unapata dozi zote mbili za chanjo.

Ikiwa huwezi kuhudhuria miadi yako, panga upya haraka iwezekanavyo.

Mambo ya kuzingatia kabla ya kupata chanjo yako

Ikiwa umekuwa na athari kali au ya haraka ya mzio kwa chanjo au sindano yoyote hapo zamani, tafadhali jadili hilo na anayekupa chanjo.

Ikiwa unatumia dawa za kufanya damu kuwa nyepesi au una matatizo ya kutokwa na damu, tafadhali mjulishe anayekupa chanjo.

Ikiwa wewe ni mjamzito, tafadhali zungumza na anayekupa chanjo, daktari au mkunga wako.

Kwa sasa hatutoi chanjo ya Pfizer kwa wale walio chini ya umri wa miaka 12.

Ikiwa una dalili za COVID-19, pimwa na ukae nyumbani hadi upate matokeo yako. Unaweza kupewa chanjo mara tu utakapopata matokeo hasi.

Ni nini kitakachotokea baada ya kupata chanjo yangu?

Utahitaji kusubiri kwa angalau dakika 20 baada ya kupata chanjo yako ili wafanyakazi wa matibabu waweze kuangalia ikiwa una athari mbaya ya mzio.

Unaweza kuhitaji kuangaliwa kwa muda mrefu ikiwa umekuwa na athari kali inayotokana na chanjo au bidhaa nyingine hapo awali, au una njia ndefu ya kusafiri baada ya kupata chanjo yako.

Madhara yanayoweza kutokea

Kama ilivyo kwa dawa zote, chanjo inaweza kusababisha madhara kwa baadhi ya watu. Haya ni ya kawaida, kawaida huwa sio kali na hayadumu kwa muda mrefu na hayatakuzuia kupata kipimo cha pili au kufanya shughuli zako za kila siku.

Athari zilizoripotiwa sana ni maumivu mahali ambapo sindano imedungwa, maumivu ya kichwa na kuhisi uchovu.

Maumivu ya misuli, kujihisi mgonjwa, baridi, homa, maumivu ya viungo na kichefuchefu pia kinaweza kutokea. Hii inaonyesha kuwa chanjo inafanya kazi. Madhara haya yanaripotiwa zaidi baada ya kipimo cha pili.

Madhara mengine yanaweza kuathiri kwa muda mfupi uwezo wako wa kuendesha au kutumia mashine.

Athari mbaya za mzio hufanyika lakini ni nadra sana. Watoa chanjo wamefundishwa kuzidhibiti.

Usaidizi na maelezo zaidi

Ukipata dalili ambazo zinaweza kuwa zinahusiana na COVID-19, kukohoa kwa muda mrefu, halijoto ya juu/homa au upotezaji au mabadiliko katika hisi yako ya kawaida ya ladha au kunusa, kaa nyumbani na upimwe COVID-19.

Ikiwa huna uhakika kuhusu dalili zako au ikiwa zinaendelea kuwa mbaya, piga simu kwa 0800 358 5453.

Ikiwa una wasiwasi wa dharura kuhusu usalama wako, piga simu kwa 111, na hakikisha umewaambia umepata chanjo ya COVID-19 ili waweze kukutathmini vizuri.

Ni muhimu kupata maelezo sahihi

Fahamu maelezo yasiyo sahihi kwenye mitandao ya kijamii na maeneo mengine.

Unaweza kupata maelezo sahihi na ya kuaminika kwenye:

covid19.govt.nz/vaccine

health.govt.nz/covid-vaccine (external link)

au piga simu kwa 0800 358 5453.

Last updated: